Madini mapya yamegunduliwa nchini Tanzania, katika eneo lenye madini ya kipekee la Manyara, na kupewa jina Merelaniite. Jina
hilo limetokana na eneo ambalo madini hayo yalipatikana, Merelani
(Mererani) katika milima ya Lelatema katika wilaya ya Simanjiro katika
eneo la Manyara. Eneo hilo linafahamika sana kwa madini ya Tanzanite. Madini
hayo yaligunduliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha
Michigan cha Marekani, makavazi ya historia asilia ya London, chuo kikuu
cha Di Firenze cha Italia na makavazi ya historia asilia ya Smithsonian
ya Washington.Wataalamu sita waliofanya uchunguzi, kwenye makala
iliyochapishwa kwenye jarida la Minerals (Madini) wanasema madini hayo
yana vipande vinavyofanana na sharubu vya rangi ya kijivu vya urefu wa
milimita moja hivi, ingawa kuna baadhi vyenye urefu wa hadi mililita 12. Kipenyo cha vipande hivyo ni mikrometa kadha. Madini
hayo yanakaribiana na madini ya zoisite (aina ya tanzanite), prehnite,
stilbite, chabazite, tremolite, diopside, quartz, calcite, graphite,
alabandite na wurtzite.
"Madini
haya mapya yametambuliwa na taasisi inayoyapa majina madini, IMA CNMNC
(2016-042), na kupewa jina linalotokana na eneo yalipogunduliwa kwa
heshima ya wachimba migodi wa eneo hilo wa zamani, wanaoishi na
wanaofanya kazi," makala ya wataalamu hayo inasema. "Wilaya ya
Merelani imekuwa maarufu tangu mwishoni mwa miaka ya 1960 kutokana na
aina ya madini ya thamani ya rangi ya samawati kwa jina zoisite
yafahamikayo kama tanzanite, lakini ni eneo muhimu sana kwa wanaotafuta
madini ya kipekee na ni eneo la kusisimua sana kutafuta madini mapya,"
John Jaszczak, mwanafizikia katika Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha
Michigan, na aliyeongoza katika kuandika makala kuhusu ugunduzi wa
madini hayo anasema. Madini hayo yalitambuliwa mara ya kwanza
mwaka 2012 na Simon Harrison na Michael Wise, bila wataalamu hao
kuyafahamu vyema, pale walipogundua vitu vilivyoonekana kama nyaya ndogo
zilizokuwa zimedunga na kuingia ndani ya vipande vya madini ya
chabazite. Baadaye uchunguzi zaidi ulifanywa na ikagunduliwa kwamba yalikuwa madini tofauti.
No comments:
Post a Comment